Shirika la Maktaba za Vyuo Vikuu na Taasisi zinazofanya Utafiti Tanzania (COTUL) limeiomba Serikali kupitia ofisi ya Waziri Mkuu kusaidia kununua machapisho ya kielektroniki yanayotumika kufundishia vyuoni kwa kuwa yanauzwa bei ghali ambayo shirikisho hilo haliwezi kumudu kuyanunua.
Mwenyekiti wa Shirikisho hilo, Dkt. Sydney Msonde alitoa ombi hilo Novemba 09, 2023 wakati wa ufunguzi wa kongamano la kisayansi ambalo limewakutanisha wanataaluma mbalimbali katika ngazi ya wakutubi, walimu wafundishaji kutoka vyuo vikuu Tanzania Bara na Visiwani, watafiti pamoja na watu wanaoshughulika na masuala ya teknolojia.
Dkt. Msonde ametoa mfano uchapishaji wa kanzi data inayoitwa Science Direct ambayo inauzwa dola za Marekani 250,000 hivyo sio rahisi kwa taasisi moja za hapa nchini kuweza kumudu kununua chapisho kama hilo.
"COTUL kazi yetu kubwa ni kuhamasisha na kuzileta pamoja taasisi zote za umma na za watu binafsi ili ziweze kuchangia kwa sehemu rasilimali fedha zitakazo wezesha kununua machapisho hayo ya msingi katika kukidhi haja ya kufanya ufundishaji na utafiti nchini." — Dkt. Sydney Msonde, Mwenyekiti wa COTUL
Mkurugenzi wa Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini Ofisi ya Waziri Mkuu, Sakina Mwinyimkuu, alipongeza COTUL kwa kupiga hatua kubwa katika kipindi cha miaka 15 tangu shirikisho hilo lilipoanzishwa mwaka 2008, na akasisitiza kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono kazi za COTUL.
Mkurugenzi wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB), Dkt. Mboni Ruzegea, alisema Serikali ya awamu ya sita inafanya maboresho makubwa ya maktaba kutoka mfumo wa kizamani wa karatasi kwenda mfumo wa kidijitali.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Totoo Ltd, Dkt. Elvis Silayo, alisema changamoto kubwa inayofanya watu wengi washindwe kuitumia maktaba ni kutojua taarifa wanazoweza kuzipata — na kwamba maktaba za kisasa zinapaswa kuwa na taarifa zinazokwenda na wakati.
Baadhi ya wadhamini wa kongamano: Totoo Company Ltd, EBSCO, Elsevier, JoVE, BUKU, Eclat, Bookstore, Emerald Insight, TCC, na LexisNexis.